SHORT STORIES

SEHEMU YA KWANZA
Simulizi: JUMBA LA LAANA (01)
Mtunzi: KINGO .INC
Simu: 0654608832

“Hodi hodi wenyewe!”. Nilizidi kuligonga geti la jumba hili huku nikiipaza sauti yangu pasi kupata majibu. 
“Jamani wenye nyumba hodiiiiiii!”. Niliendelea kubisha hodi pasipo kukata tamaa. 
Sikutaka kukata tamaa kabisa kwani niliamini ya kwamba wakazi wa jumba hili la kifahari ni lazima watakuwepo ndani tu. 
Pia nilikuwa nimekwishachoka kwa mida hii ya jioni kwani nilikwishazunguka sana katika viunga vya jiji hili la Kano mchana kutwa pasi kufanikiwa kwa matakwa yangu.
Nilikuwa nikijiandaa kuligonga geti la jumba lile la kifahari kwa mara nyingine tena lakini nikasita mara baada ya kusikia mlio wa geti kujulisha kwamba kuna mtu ambaye alikuwa akilifungua. 
Baada ya geti kufunguliwa, macho yangu yalipigwa na bumbuwazi na kubabaika kwa sekunde kadhaa huku nikijilambalamba midomo yangu. 
Mbele yangu alisimama mama mmoja wa makamo ambaye alikuwa na uzuri na urembo usiomithilika.
“Shikamoo mama!”. Ilinitoka salaamu hii katika kinywa changu. 
“Eeee bwana eeeeh! Acha kunizeesha!”. Alijibu mama yule mrembo wa makamo mara baada ya kuushusha msonyo mkali sana wa dharau. 
“Naomba radhi kwa hilo”. Niliamua kuwa mpole na kuomba radhi baada ya kugundua kwamba huyu mama alikuwa na dharau sana.
“Haya sema shida yako upesi maana wanitia kinyaa”. Yule mama aliongea huku akiibinua midomo yake kwa dharau. 
“Samahani, shida yangu ni kwamba ninatafuta kazi”. Niliongea kwa woga kidogo. 
“Ha ha ha haaaaaaa! Hebu rudia tena”. Yule mama aliongea mara baada ya kukishusha kicheko kikali. 
“Nimese …..se….sema naomba kazi”. Nilirudia kauli yangu lakini sasa hivi ni kwa kubabaika sana. 
“Enheeeeeeeee! Wataka kazi gani wewe?”. Yule mama aliuliza. 
“Kazi yoyote mama yangu”.
“He! Wewe nishakuambia usinizeeshe. Hivi ni kwa nini husikii?”. Yule mama alilalama. 
“Naomba radhi kwa hilo”. Niliongea. 
“Haya hebu jitazame toka juu mpaka chini. Hivi unaona ya kwamba wewe una hadhi ya kupata kazi katika nyumba hii?”. Mama alihoji. 
Nilijitazama toka juu mpaka chini kama nilivyotakiwa. Niligundua kwamba nilikuwa sistahili kabisa hata kulisogelea jumba hili.
“Mama mpe kazi”. Ilikuwa ni sauti tamu na nyororo iliyofuatiwa na mrembo wa haja ambaye alikuwa na uzuri wote mithili ya malaika. 
Moyo wangu ulipigwa na butwaa kwani katika maisha yangu sikuwahi kumwona mwanamke mzuri kama huyu. Niliamini kwamba hakika nyumba hii ilibarikiwa kuwa na wanawake warembo sana. 
“Unasemaje Catherine?”. Yule mama alihoji. 
Hapo ndipo nilitambua kwamba yule mrembo uliotukuka mithili ya malkia wa Sheba mbele yangu alikuwa akiitwa Catherine. 
“Tumwajiri mama kwani yule kijana wa kuhudumia maua ameacha kazi na mazingira yameanza kuwa mabaya”. Catherine aliongea kwa kujiamini. 
“Sasa na uchafu wake huu mithili ya nguruwe pori tutamlaza wapi?”. Yule mama alihoji kwa dharau ambayo ilimfanya nitiririkwe na machozi. 
“Sehemu ya kulala itapatikana tu”. Catherine alizidi kunitetea niajiriwe. 
“Haya basi mimi nakuachia huyo nguruwe. Namna ya kumhudumia utajua wewe. Na asithubutu kuingia sebuleni asije akatia shombo”. Mama Catherine aliongea huku akiondoka na kumwacha nikiwa na Catherine. 
“Pole sana. Msamehe sana mama yangu kwani hivi ndivyo alivyo”. Catherine aliongea na kunishika mkono na kuingia ndani bila kujali hali ya ufukara niliyokuwa nayo. 
Nilishangaa sana pindi nilipoingia ndani ya jumba lile. Lilikuwa ni jumba safi na nadhifu sana ambalo katu katika maisha yangu sikuwahi kuingia.
“Ama kweli watu wanaishi kama wako paradiso”. Niliwaza moyoni mwangu. 
“Haya ndiyo maua ambayo utakuwa ukiyahudumia. Hakikisha kwamba hayanyauki”. Catherine aliongea akinionyesha mazingira huku akiwa amenipokea mzigo wangu. 
“Na hiki ndicho kitakuwa chumba chako cha kulala. Choo na bafu viko humohumo ndani”. Catherine aliongea.
“Kwa sasa nenda kaoge kisha upumzike”. 
“Ahsante sana Catherine”. Niliongea kumshukuru Catherine. 
Kuna kitu kilimshtua Catherine katika sauti yangu. Ilikuwa ni sauti tamu ambayo ilikuwa na mvuto nadhifu sana. Alipenda jinsi nilivyolitamka jina lake. 
“Usijali kaka. Sijui waitwa nani vile?”. Catherine alihoji. 
“Mimi naitwa Ibrahim”. 
“Ok, Ibrahim, tutaonana baadaye”. Catherine aliongea.
“Ok, usijali dada Catherine”. Nilijibu huku nikimtazama Catherine ambaye alikuwa akiondoka kwa mwendo wa pozi sana.
Mimi niliingia ndani ya ile chumba ambacho nilielekezwa kwamba kitakuwa ndicho chumba change. Nililiweka begi langu ndani ya kabati la nguo na kisha nikakaa na kuishusha pumzi moja ndefu ya furaha ambayo ilichanganyikana na kukata tamaa.
“Hivi kweli nitayaweza maisha ya hapa maana yule mama mwenye nyumba anaonekana ni mshari sana”. Niliyapitisha mawazo hayo huku macho yangu nikiwa nimeyaelekeza juu ya dari.
“Lakini huyu Catherine anaonekana ni mtu mzuri kabisa mwenye moyo wa huruma kwani bila yeye kazi hii nisingeipata. Itanibidi nifanye kazi kwa bidii ili kuwafurahisha hawa waajiri’. Niliendelea kuwaza.
“Ngoja niende kuoga ili niuondoe uchovu pamoja na mawazo niliyonayo”. Niliwaza hayo huku nikisimama na kuelekea katika bafu lililokuwa mle ndani.
Baada ya kuoga na kujipaka mafuta nilijilaza juu ya kitanda na kupitiwa na usingizi kutokana na uchovu mkubwa niliokuwa nao. 
*****************
Tukutane katika sehemu ya 02 ya kisa hiki cha kusisimua
************************************************************************
***********************************************************************

 1. SEHEMU YA PILI
  Simulizi: JUMBA LA LAANA (02)
  Mtunzi:KINGO .INC
  Simu: 0654160231

  ILIPOISHIA
  “Ngoja niende kuoga ili niuondoe uchovu pamoja na mawazo niliyonayo”. Niliwaza hayo huku nikisimama na kuelekea katika bafu lililokuwa mle ndani.
  Baada ya kuoga na kujipaka mafuta nilijilaza juu ya kitanda na kupitiwa na usingizi kutokana na uchovu mkubwa niliokuwa nao.
  SASA ENDELEA
  Nilishtushwa kutoka katika usingizi mzito niliokuwemo kutokana na sauti ya mlango uliokuwa ukigongwa. Nilikurupuka kifua wazi na kwenda kuufungua mlango ule.
  Nje kulikuwa na mwanga ambao ulitokana na taa za umeme. Hii ilijulisha kwamba kiza kilikuwa kimeingia. Pia ilimaanisha kwamba nilikuwa nimelala kwa muda mrefu toka nilipokuwa nimetoka kuoga.
  Macho yangu yalipigwa na butwaa baada ya kukutana na msichana mzuri na mrembo ambaye baadaye nilikuja kufahamu kwamba alikuwa ni mtumishi wa ndani na jina lake aliitwa Lydia.
  Yaani niliishangaa sana nyumba hii kwa kubwarikiwa kuwa na wasichana warembowarembo tu. Yaaani ilikuwa mithili ya jumba la kifalme ambalo limepambwa na wanawali wengi warembo.
  Macho ya Lydia ambaye alikuwa ameshika sinia lenye hotpots na sahani yalitua katika kifua change. Nilikuwa na kifua chenye mvuto ambacho kilikuwa kimejazia kimazoezi. Lydia alijilamba midomo kwa matamanio huku macho yake yakiwa yamejawa soni.
  “Dada Cathy kanambia nikuletee chakula”. Lydia liongea kwa sauti yenye mvuto wa kuweza kumtoa nyoka pangoni.
  “Ahsante sana nashukuru”. Nilimjibu Lydia kwa sauti ambayo ilimvutia sana na kumfanya afunge macho kwa raha.
  “Naitwa Lydia”. Aliniambia pindi akinikabidhi chakula.
  “Ahsante sana. Nashukuru kukufahamu. Mimi naitwa Ibrahim”. Nami nilimjibu Lydia.
  “Ahsante Ibrahim. Karibu sana”. Lydia alijibu huku akiondoka na kunirembulia macho.
  Nilimtazama kwa nyuma Lydia na kujilamba midomo yangu. Alikuwa na makalio makubwa kiasi ambayo yalikuwa yakitetemeka pindi alipokuwa akitembea. Kiuno chake kilikuwa ni chembamba ambacho kilimwongezea urembo usio kifani.
  Niliingia ndani pamoja na kile chakula ambacho nilikuwa nimepewa. Nilikiweka juu ya meza moja ndogo iliyokuwamo katika chumba kile. Niliyafunua mabakuli yale na kukutana na chakula kizuri sana ambacho kilinipa hamu kunwa sana ya kula.
  Ulikuwa ni wali uliotoa harufu nzuri sana. Bakuli jingine lilikuwa limesheheni nyama za kuku ambazo nazo zilinitoa udenda. Nilikwishasahau kwa mara ya mwisho nilikula lini chakula kama hiki.
  Sikutaka kuupoteza muda hata kidogo. Nilikivamia kile chakula na kuanza kukishughulikia. Nilikula mpaka pua zangu zikatoa jasho kuonesha kwamba nilikuwa nimeshiba sana. Kwa wakati huo pia tumbo langu lilikuwa limejaa ndiiii! huku midomo yangu ikisaidia kubeua kwa shibe.
  *************
  Kesho yake nilijihimu alfajiri ya saa kumi na moja na kuanza kuyashughulikia maua ambayo yalikuwa katika hali mbaya kabisa. Niliyalisha maji ya kutosha. Kisha nikaanza kuyatifulia ili kuondoa magugu.
  Kufikia saa moja na nusu ya asubuhi maua yote yalikuwa yakipendeza kwa kupewa maji na kuondolewa magugu.
  Baada ya kumaliza kazi hii ambayo ilinitoa jasho, sasa nikaanza kuufagia uwanja wote wa nyumba ile ambao nao ulisahauliwa katika kufanyiwa usafi.
  Baada ya kumaliza kuufagia, nilichukua jembe na fyekeo na kutoka nje ya jumba lile. Nikaanza kufyeka majani na kukwangua mengine. Shughuli hii ilinichukua mpaka saa sita na nusu. Jumba lote sasa lilikuwa linang’ara kwa usafi.
  Baada ya kujihakikishia kwamba nimeyatimiza majukumu yangu vema, nikachukua vifaa vyangu vya kufanyia usafi na kuanza kurejea ndani. Na kwa wakati huo nilikuwa katika mapigo ya singlend na suruali aina ya tracksuit.
  “Ibrahim, umefanya kazi yote hii?”. Ilikuwa ni sauti ya Catherine ikinilaki mara baada ya mimi kuingia katika geti kubwa la kuingilia jumba lile.
  “Mh! Mbona kawaida tu”. Nilimjibu Catherine kwa sauti yangu ile nzito yenye mvuto.
  “Duh! Yaani jumba lote saa hizi linang’ara. Hongera sana Ibrahim”.
  “Usijjali dada Cathy, ngoja mimi nikaoge”. Nilimwambia Catherine ambaye sasa macho yake yalikuwa yametua katika kifua change na alijilamba ulimi kwa matamanio.
  “0k, vipi umekwishakunywa chai?”. Catherine aliniuliza.
  “Hapana sijanywa bado kwani toka niamke alfajiri nimekuwa nimetingwa na kazi” Nilimjibu Catherine.
  “Oooh! Jamani, pole sana. Lydiaaaaaa….!”. Catherine aliita.
  “Abeeee! Dada”. Lydia aliitika toka ndani.
  “Hebu mwandalie kaka chai”. Catherine aliongea.
  “Sawa, naileta sasa hivi”. Lydia alijibu tena toka ndani.
  Mimi nilienda kuviweka vile vifaa vya usafi mahali ambapo panatakiwa kisha nikaenda ndani kwangu kwa lengo la kuoga.
  **************
  Muda uliendelea kusonga mbele huku nami nikiwa sasa nimeyazoea mazingira ya jumba hili kwa kiasi kikubwa. Niliyabadilisha mazingira yale na kulifanya jumba ling’are kwa unadhifu.
  Jambo ambalo lilikuwa likinishangaza katika jumba hili ni kwamba, toka nimefika yapata mwezi sasa sijawahi kumwona baba mwenye nyumba. Sikutaka kulihoji hili kwani lilikuwa halinihusu hata kidogo. Niliendelea kuchapa kazi.
  Damu yangu na mama yake Catherine naona haikupatana kabisa. Kwani kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo alizidi kunichukia. Sikufahamu kwa nini kwani mimi nilikuwa ni kijana mpole nisiyependa makuu na mtu yeyote.
  “We mwehu, hivi kwa nini umekaa hapa? Ina maana umekosa kazi za kufanya”. Mama Caherine aliongea siku moja pindi aliponikuta nimekaa katika bustani ya maua ya jumba lile.
  Wakati huo ilikuwa ni mchana na kwa kuwa nilikuwa nimekwisha maliza kazi zangu, niliona ni bora nijipumzishe kidogo pale bustanini kwa kupunga upepo.
  “Nimekwishamaliza kazi zanu mama!”. Nilimjibu yule mama huku nikiwa nimeshtuka kweli.
  “Hautakiwi kukaakaa kizembe humu ndani. Hebu chukua ufagio na anza kufagia uwanja”. Yule mama aliongea.
  “Nilikwishafagia uwanja wote na pia bado ni msafi kama unavyouona mama”. Nilimjibu yule mama.
  “Ina maana wewe unabishana na mimi eeeh!? Halafu nilikwishakukukataza kuniita mimi mama. Usipende kunizeesha”. Yule mama alibwata.
  “Nisamehe sana”. Nilijibu huku nikisimama na kwenda katika banda la kuhifadhia vifaa vya kazi. Nikauchukua ufagio na kisha nikaanza kufagia.
  ***********
  “He, Catherine hii nyumba mbona siku hizi inang’ara sana?”. Ilikuwa ni sauti nzito ya kiume ikiunguruma asubuhi hii ya leo.
  Kwa wakati wote huu mimi nilikuwa bustanini nikiwa nimetingwa na umwagiliaji wa maua. Nilikuwa naipenda sana kazi yangu hii na niliifanya kwa dhati.
  “Kuna kijana tumemwajiri ambaye anatusaidia kazi hizi za usafi wa mazingira baba”. Catherine alijibu.
  “Naweza kumwona maana yaonesha ni kijana mchapakazi sana”.
  “Ndio baba. Ngoja nikupeleke. Yuko kule bustanini”.
  Catherine na yule mzee waliongozana mpaka kule bustanini ambako nilikuwa nikifanya kazi ya kuyalisha maua chakula chake.
  “Habari yako kijana?”.
  “Mziri tu mzee wangu. Shikamoo”. Niliitoa salamu ya unyenyekevu iliyojaa staha kubwa.
  ‘Ninaitwa mzee Chitenge. Ndiye baba mwenye nyumba hii”. Aliongea yule mzee wa makamo.
  “Ahsante sana. Nashukuru kukufahamu. Mimi naitwa Ibrahim”. Nami nilijitambulisha kwa yule mzee.
  “Mazingira ya kazi unayaonaje?”. Mzee Chitenge aliuliza.
  “Yako vizuri kabisa mzee wangu. Hakuna tatizo lolote”. Nilijibu.
  “Kama kuna tatizo usisite kututaarifu”. Mzee Chitenge aliongea.
  “Usijali mzee wangu”. Nilimjibu.
  “Ok, karibu sana na nikuache uendelee na kazi”. Aliongea mzee Chitenge.
  “Ahsante sana. Nashukuru mzee wangu”. Nilijibu.
  Mzee yule aliondoka na Catherine huku wakiendelea kuongea mawili matatu kwa furaha na bashasha.
  Huyu mzee alionekana ni mzee mkarimu ingawa nilikuwa sijapata kumfahamu hapo kabla. Nilihisi hivyo kutokana na upole na ucheshi wake. Niliifurahia tabia ya huyu mzee.
  ***********
  Tukutane katika sehemu ya 03 ya kisa hiki cha kusisimua