June 20, 2016

Upepo wa kuto aminiana BUNGENI.

WAKATI Bunge likitarajiwa kupitisha Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais John Magufuli kesho, bila uwepo wa Kambi ya Upinzani,tathmini ya baadhi ya matukio yaliyoanza kuongezeka kutoaminiana kati ya kambi hiyo na uongozi wa Bunge, hasa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Ingawa taarifa nyingi zimekuwa zikieleza kuwa Dk Tulia ndiye mbabe, taarifa za uendeshaji wa shughuli za Bunge tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zinaonesha namna wabunge wa Ukawa, walivyoonesha kutojali heshima ya chombo hicho na viongozi wake.

Taarifa hizo za Bunge zilizopitiwa na gazeti hili wiki hii, zimeonesha bila kuacha shaka namna baadhi ya wabunge wa kambi hiyo, wanavyodharau Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mtu yeyote aliyekalia Kiti cha Spika, achilia mbali Dk Tulia ambaye ndiye anayetajwa zaidi kuwa mbabe.

Mbali na dharau kwa Bunge na viongozi wake, wabunge hao wameonesha namna walivyotayari kutumia ubabe ndani ya Bunge ikibidi kupigana, huku wengine wakitumia uongo kwa nia ya kuichafua serikali na viongozi wake kwa umma.

Dharau za Bulaya

Mbali na matukio ya mara kwa mara na ya kawaida ya wabunge hao wa Ukawa kukaidi agizo la kutakiwa kukaa chini au kukaa kimya kutoka kwa aliyekalia Kiti cha Spika, ambaye ndiye anakuwa na Mamlaka ya Spika, dharau kubwa iliyosikitisha viongozi wa Bunge, ilioneshwa na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya.

Mbunge huyo baada ya kuonekana kushiriki kufanya vurugu Januari 27, 2016 wakati wabunge hao wa Ukawa walipozuia shughuli za Bunge za mchana na jioni kutofanyika kwa kusimama na kupiga kelele mfululizo, yeye na watuhumiwa wenzake walitakiwa kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kutoa maelezo kuhusu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.

Watuhumiwa wengine walioitwa mbele ya kamati hiyo Machi 9 mwaka huu, kwa kutumia hati ya wito yenye nguvu sawa na ya Mahakama, ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu; Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul. Pamoja na kuthibitisha kuwa Bulaya na watuhumiwa wenzake walipokea hati hiyo, ni mbunge huyo pekee wa Bunda ambaye hakufika na wala hakuona umuhimu wa kutoa taarifa yoyote ya kutofika kwake.

Kwa kutumia nguvu ya kisheria ya kamati hiyo ambayo ina hadhi sawa na ya kimahakama, Kamati hiyo ililazimika kumwandikia Spika barua kumjulisha, kuhusu hatua ya Bulaya kukaidi wito wa kamati.

Kukamatwa kwa Bulaya

Spika wa Bunge, Job Ndugai, hakuwa na namna bali kutoa kibali chake cha kukamatwa kwa Bulaya, kilichokabidhiwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na polisi walifanya kazi yao, walimkamata Mbunge huyo akiwa katika Hoteli ya Gold Crest, Mwanza.

Akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, Bulaya alipandishwa ndege na kupelekwa jijini Dar es Salaam Machi 11, 2016 kwenda kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Utetezi wa Bulaya

Taarifa za Bunge zinaonesha Bulaya alipewa fursa ya kujitetea kwa nini hakutii wito wa Kamati ya Bunge, kama walivyofanya watuhumiwa wenzake ambao nao ni wabunge kama yeye, ambapo mbunge huyo alitoa utetezi wa aina mbili uliokuwa ukipingana.

Kwanza Bulaya alidai kuwa alikuwa anaumwa na kwamba kwake yeye suala la afya yake, lilikuwa muhimu zaidi kuliko kutii wito huo wa kamati. Katika utetezi wa pili alioutoa baada ya Kamati hiyo kumdadisi, alijikuta akiacha hoja ya ugonjwa na kukiri kuwa alikuwa Mwanza kuhudhuria mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema, kama mjumbe mwalikwa.

"Kamati ilisikitishwa na kitendo cha Mheshimiwa Bulaya kudharau wito wa Kamati," taarifa rasmi za Bunge zimemnukuu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM).

Dharau zaidi, busara ya Bunge Pamoja na Lema, Lissu na Gekul kutii wito wa kwanza ambao Bulaya alikaidi, katika tukio lililoonesha dharau nyingine kwa Bunge, ni pale wabunge hao waliotii wito wa kwanza walipoomba kupewa muda ili washauriane na mawakili wao, kabla ya kujibu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.

Kwa busara, Kamati hiyo iliamua kuwapa wabunge hao haki yao ya kusikilizwa iliyotimia kwa kuwapa muda wa siku mbili zaidi, ili wawasiliane na kupata ushauri wa mawakili ambapo walitakiwa kurudi katika Kamati Machi 11, 2016 ili kujibu tuhuma zao baada ya kupata ushauri wa mawakili.

"Kamati iliamua kutoa fursa kwa mashahidi walioomba kupewa fursa ya kupata mawakili. Mashahidi hao ni Tundu Lisu, Godbless Lema na Pauline Gekul. Kamati iliwapa muda wa siku mbili toka Machi 9 hadi Machi 11, 2016 ili kuwawezesha kupata mawakili kama walivyoomba," ilieleza taarifa hiyo ya Bunge.

Katika tukio linaloonesha dharau 'iliyopangwa' kwa Bunge, wabunge hao watatu waliamua kutofika kati tarehe waliyokubaliana kuwa wangefika mbele ya Kamati na hawakuwahi kuwasilisha maelezo yoyote mbele ya Kamati, kuhusu sababu za kushindwa kufika.

Busara ya Kamati hiyo, haikuelekeza kutumia kibali cha kuwakamata, bali ilielekeza kwamba kwa kuwa walipewa fursa ya kutosha ya kusikilizwa na walifahamishwa kuwa wakishindwa kufika, kamati itaendelea na kazi zake, Kamati hiyo ikaendelea kujadili tuhuma zao bila kupata utetezi wao.

Ubabe

Wakati anayetajwa zaidi kwa ubabe ni Dk Tulia, lakini wabunge hao wa Ukawa na hata Kabwe Zitto wa ACT, mbali na kuonesha dharau iliyolazima viongozi wa Bunge kutumia busara kuwa nao, wamekuwa wakitumia ubabe na kelele zenye lengo la kuzuia Bunge kufanya shughuli zake na dhidi ya aliyekalia Kiti cha Spika.

Ubabe wa hali ya juu uliowahi kuoneshwa ndani ya Bunge hilo, ulifanywa na Lema, ambaye aliwahi kabisa kuvua koti na tai tayari kupigana, huku akisema yuko tayari kuuawa akigombea haki.

Taarifa za Bunge zinaonesha siku waliyofanya vurugu, Lema "alivua koti na tai, ikiwa ni ishara ya kujiandaa kupigana, jambo ambalo halitegemewi kufanywa na kiongozi wa hadhi ya Mbunge.

"Mimi wataniua, hapa tunagombea haki," alisikika Lema akisema huku amevua koti na tai hatua ambayo imetafsiriwa kuwa "utovu wa nidhamu wa hali ya juu kwa Mamlaka ya Spika ambao haupaswi kuvumiliwa kwa vyovyote vile…" Mbali na Lema, Zitto alionekana akipiga kelele na kubishana na Spika mfano: Spika: Naomba waheshimiwa mkae.

Zitto: (Akikaidi agizo la Spika) Mheshimiwa Spika, Hoja ya hadhi ya Bunge. Spika: Naomba sana mkae, naomba nichukue nafasi hii kumkaribisha Mwenyekiti, Mheshimiwa Andrew Chenge, ili aendelee na ratiba iliyoko mezani. Mheshimiwa Chenge.

(Anaita Spika) (Makofi).

Zitto: (Akitumia ubabe) Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kuahirisha mjadala… Mwenyekiti: Mheshimiwa Zitto nakusihi sana, hiyo Kanuni ya Haki za Bunge, hailazimishi Kiti kukubali kama ilivyo, nakusihi isome vizuri. (Makofi).

Zitto: Kanuni ya 69 hoja ya kuahirisha mjadala Mheshimiwa Mwenyekiti. Taarifa za Bunge zinaonesha kuwa matukio kama hayo yamefanywa pia na Mdee na Lissu, ambaye wakati fulani alikuwa akihamasisha wabunge wote wa Ukawa wasimame, wakati aliyekalia Kiti cha Spika, amekataza.

Lissu: Mwongozo wa Mwenyekiti… Simameni basi.

Mwenyekiti: Ni mwongozo tu, wote mnataka mwongozo?

Wabunge wengi: Ndiyo.

Mwenyekiti: Unafanana na hili alilosema Mheshimiwa Heche?

Lissu: Si mnataka mwongozo, simameni muombe mwongozo.

Mwenyekiti: Waheshimiwa wabunge, naona sasa tunataka kutumia utaratibu wa kuchelewesha shughuli za Bunge.

Lissu: Mwongozo, mwongozo, tunataka mwongozo. Mwenyekiti: Nimesimama (Kanuni inataka wote wakae).

Lissu: Mwongozo (anakaidi).

Mwenyekiti: Nimesimama. (Akisihi). Matumizi ya uongo Mbali na dharau, vurugu na ubabe juzi taarifa nyingine ya Bunge iliwashika wabunge wa Viti Maalumu wa Ukawa, Susan Lyimo na Anatropia Theonest kwa kusema uongo.

Susan alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mei 11 mwaka huu, alidai kuwa Serikali imenunua magari 777 ya 'washawasha', ambapo alidai kuwa ni magari 50 tu yaliyotumika kwenye uchaguzi.

Alipotakiwa kufuta kauli alionesha kuwa anao ushahidi, alipotakiwa kuupeleka, alitumia ushahidi aliodai ni wa Mwananchi Online, taarifa rasmi za Bunge, taarifa za mtandao wa Alibaba na kielelezo kutoka Habarikablog. blogspot.com. Hata hivyo vielelezo hivyo, vilipofanyiwa uchambuzi hakukuwa na kielelezo cha Mwananchi Online, bali cha Mwanahalisi Online na pia kielelezo cha Habarikablog. blogspot.com hakikuainishwa.

Pili hakukupatikana kielelezo hata kimoja kilichothibitisha kuwa Serikali imenunua magari hayo 777 ya 'washawasha'. Anatropia Anatropia yeye katika kusema uongo, alidai bungeni kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa Mkuu wa Mkoa mwaka 2011, alihusika na uporaji wa maeneo ya wananchi yaliyopo Tegeta.

Mbunge huyo wa Ukawa alidai kuwa maeneo yaliyoporwa na Lukuvi, yalikuwa ya wananchi waliokuwa wakiishi mabondeni, wakiwemo wa Jimbo la Segerea na wananchi wa Ilala, ambao sasa wanataka maeneo yao huku wakidai kuwa Lukuvi alihusika kuyapora.

Kutokana na uongo huo, Lukuvi alilalamika kuwa mwaka 2011, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge na si Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na wala hakuhusika na tuhuma hizo.

Katika malalamiko yake, taarifa za Bunge zinaonesha kuwa Lukuvi alisema tuhuma zilizotolewa na Anatropia, si tu kwamba zilikuwa za uongo, bali pia zimemfedhehesha kwa kumhusisha na uporaji wa viwanja vya watu wanyonge.

Akiri ni muongo Alipoitwa Anatropia taarifa za Bunge zinaeleza; "alikiri mbele ya Kamati kuwa alisema uongo bungeni kwa kuwa ni kweli Lukuvi hakuwa Mkuu wa Mkoa mwaka 2011, hivyo asingeweza kuhusika na uporaji wa viwanja vya waathirika wa mafuriko."

Anatropia ameelezwa katika taarifa hiyo kuwa, iwapo angeambiwa jambo hilo akiwa bungeni, kuwa kauli aliyokuwa ameitoa siku hiyo ilikuwa ya uongo angeifuta.

Kutokana na vitendo hivyo, ingawa wabunge wa Ukawa wanasema Bunge linaongozwa kibabe, lakini ilibidi Bunge litoe adhabu mbalimbali za kinidhamu kwa wabunge saba wa Ukawa na Zitto wa ACT. Mbali na Zitto, wengine waliopewa adhabu ni Susan, Anatropia, Lema, Heche, Mdee, Gekul na Bulaya.